Umilisi wa Stadi za Maamkizi Katika Ujifunzaji wa Kiswahili
Loading...
Date
2015-01-22
Authors
Ngugi, Boniface Mwangi
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulidhamiria kuchunguza umilisi wa stadi za maamkizi na changamoto zinazowakumba wanafunzi wa shule za upili wanapoamkuana kwa Kiswahili. Zaidi ya hayo, utafiti ulilenga kubainisha chanzo na athari za changamoto za maamkizi zinazowakumba wanafunzi wanapowasiliana katika Kaunti ya Nairobi. Umilisi wa stadi za maamkizi ni ujuzi wa kuamkuana kwa ufasaha na kwa njia inayoridhisha miktadha ya kijamii na kimawasiliano. Umilisi wa stadi za maamkizi ni jambo linalothaminiwa sana katika ulimwengu wa sasa. Bila umilisi huu, maamkizi yanaweza kumwaibisha msemaji licha ya kuwa sanifu kisarufi wakati wa mawasiliano. Utafiti huu ulichochewa na swala kuwa Baraza la Mitihani Nchini Kenya katika ripoti zake limedokeza kwamba kiwango cha wanafunzi cha umilisi wa stadi za maamkizi kimeshuka sana. Zaidi ya hayo, kila jamii ina kaida na masharti yanayotawala matumizi ya lugha na kwamba mawasiliano hutofautiana na hutegemea muktadha mpana wa jamiilugha. Mwelekeo wa utafiti huu uliibua maswala matatu muhimu: uchanganuzi wa lugha kwa misingi ya ujifunzaji, jamii, na umilisi mawasiliano. Kutokana na misingi hii, utafiti huu ulijikita katika mtazamo wa nadharia ya Mulishi kama ilivyopendekezwa na Krashen ili kukidhia swala la ujifunzaji lugha. Nadharia ya Mulishi ya Krashen hufafanua taratibu zinazotumika mwanafunzi anapopata na kujifunza lugha ya pili. Zaidi ya hayo, utafiti ulirejelea kanuni za Tahakiki Usemi zinazodhihirisha uhusiano wa lugha na jamii. Tahakiki Usemi hutazama lugha kama kifaa muhimu katika shughuli za kijamii. Hata hivyo, kwa vile utafiti ulijikita katika uchambuzi wa matumizi halisi ya lugha, nadharia ya Mulishi na Tahakiki Usemi zilishirikiana na nadharia ya Sarufi Amilishi Mfumo. Nadharia ya Sarufi Amilishi Mfumo ni ya kiisimu ambayo huchukulia kuwa miundo ya kisarufi hushirikiana na ujuzi wa mahusiano ya kijamii. Utafiti ulijikita maktabani na nyanjani. Maktabani, kulikuwa na udurusu wa vitabu, miswada, majarida na machapisho yaliyoangazia maarifa ya Isimujamii, yaliyoandikwa kuhusu maamkizi hasa katika utamaduni wa Waswahili, nadharia na mbinu za utafiti. Nyanjani, utafiti ulifanyika katika Kaunti ya Nairobi ambapo data ilikusanywa kwa njia ya uigaji wa maamkizi na kuchanganuliwa kitarakimu na kimaelezo. Matokeo ya utafiti yalidhihirisha kuwa, baadhi ya wanafunzi wa Kiswahili wameimarika na wamekuwa wabunifu wanapoamkuana na kuitikia maamkizi ya Kiswahili kama yalivyopendekezwa na silabasi. Hata hivyo, utafiti ulibainisha kuwa wanafunzi hukumbwa na changamoto za msamiati na sintaksia wanapoamkuana na kuitikia maamkizi ya Kiswahili. Changamoto husika huwa na athari zake. Athari mbili kuu zilibainika: mtatafaruku katika mawasiliano na ukwepaji maamkizi. Hatimaye utafiti ulidhihirisha kuwa changamoto za maamkizi husababishwa na kutotambua muktadha wa kijamii, kutotambua muktadha wa kimawasiliano, mtagusano wa lugha na tamaduni nyingi, na uradidi wa maamkizi. Hatimaye matokeo ya utafiti yaliwasilishwa katika sura tano mtawalia. Matokeo ya utafiti yanaweza kutumiwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitalaa kutoa mapendekezo kwa wanaofunza Kiswahili kuwashirikisha wanafunzi kimazungumzo kwa lengo la kuinua kiwango chao cha umilisi wa stadi za maamkizi. Kuwashirikisha huku kutawasaidia kutumia maamkizi yenye adabu na heshima na kudumisha mahusiano ya kijamii.
Description
Department of Kiswahili & African Languages, 281pg. 2014, PL 8702 .N6