Taathira za kiswahili na lugha nyingine kwa uthabiti wa kiisimujamii wa lugha za mama mijini Nairobi, Kiambu na Thika: mfano wa Kikuyu
Loading...
Date
2015
Authors
Kamau, Stephen Njihia
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu ni wa kiisimujamii ulioangazia suala la mtagusano wa lugha za Kikuyu, Kiswahili, Kiingereza na Sheng miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika. Utafiti wenyewe umejikita katika kuchunguza iwapo lugha za Kiswahili, Kiingereza na Sheng zinaathiri uthabiti wa kiisimujamii wa lugha ya Kikuyu miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika. Lugha ya Kikuyu huonekana kama lugha iliyo na viwango vya juu vya uthabiti wa kiisimujamii kutokana na idadi yake kubwa ya wazungumzaji nchini Kenya. Hata hivyo, huenda lugha hii si thabiti katika mazingira mengine kama yale ya mijini miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu, ambako kuna hali ya mtagusano wa lugha na wingilugha. Utafiti huu umetathmini athari za lugha ya Kiswahili, Kiingereza na Sheng kwa uthabiti wa kiisimujamii wa lugha ya Kikuyu miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika kupitia stadi za lugha za kuongea, kusoma na kuandika kama nyenzo ya kubaini uthabiti wa kiisimujamii wa lugha ya Kikuyu. Data ya utafiti huu ilikusanywa nyanjani miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika kwa kutumia mtindo wa mbinu changamano ya utafiti. Mtindo wa mbinu changamano ya utafiti unahusu matumizi ya mbinu za kimaelezo na kijarabati kwa pamoja katika utafiti mmoja. Tulitumia hojaji za matumizi na mielekeo ya lugha na mijadala ya kimakundi ili kubaini mielekeo ya vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika kuhusu lugha ya Kikuyu ikilinganishwa na lugha za Kiswahili, Kiingereza na Sheng. Aidha, vijana hawa walihusishwa katika mazoezi ya kuongea, kuandika na kusoma katika lugha za Kikuyu, Kiswahili, Kiingereza na Sheng ili kubaini viwango vyao vya umilisi wa lugha za Kikuyu, Kiswahili, Kiingereza na Sheng. Data ya utafiti huu ilichanganuliwa kwa mujibu wa malengo ya utafiti kwa kuongozwa na mihimili ya nadharia za Uthabiti wa Kiisimujamii wa Lugha na nadharia ya Vitendo Vilivyopangwa na Vitendo Vilivyofikiriwa. Matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kupitia njia za maelezo, majedwali na chati ili kuweka wazi viwango vya umilisi wa Kikuyu walio nao vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika. Utafiti huu uliweza kubaini kuwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika wana mielekeo hasi na viwango vya chini vya umilisi wa lugha ya Kikuyu. Kutokana na mielekeo hasi na viwango vya chini vya umilisi wa lugha ya Kikuyu, utafiti huu ulibaini kuwa viwango vya uthabiti wa kiisimujamii wa lugha ya Kikuyu ni vya chini ikilinganishwa na viwango vya uthabiti wa kiisimujamii wa lugha za Kiswahili, Kiingereza na Sheng miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika. Aidha, utafiti huu ulizua tasnifu kuwa kuna mpangilio mpya wa matumizi ya lugha kitriglosia miongoni mwa vijana mijini unaohusisha lugha za Kiingereza, Kiswahili na Sheng huku lugha za mama kama vile Kikuyu zikitengwa na basi kuziweka katika hatari ya kuanza kuangamia. Utafiti huu ni muhimu katika uwanja wa isimujamii kwa
vile umetambulisha hali ya kiisimujamii ya lugha ya Kikuyu miongoni mwa vijana wa jamii ya Kikuyu mijini Nairobi, Kiambu na Thika. Tunatarajia kuwa matokeo ya utafiti huu yatasaidia katika kuanzisha shughuli za kuimarisha na kuinua viwango vya uthabiti wa kiisimujamii wa lugha za mama kwa jumla miongoni mwa vijana mijini nchini Kenya.
Description
Tasnifu ya uzamifu (phd) chuo kikuu cha kenyatta idara ya kiswahili tasnifu hii imewasilishwa katika idara ya kiswahili ili kutosheleza mahitaji ya shahada ya uzamifu katika chuo kikuu cha Kenyatta, Agosti 2015