Maudhui na Matumizi ya Lugha Katika Nyimbo za Injili za Rose Muhando

Loading...
Thumbnail Image
Date
2013-08-08
Authors
Kasau, Mue Elizabeth
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu umeonyesha jinsi ambavyo lugha imetumiwa katika kuwasilisha maudhui katika nyimbo kumi za injili za mwimbaji Rose Muhando. Nyimbo zilizoshughulikiwa zilitungwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2004 hadi 2011. Data imechunguzwa na kuchanganuliwa ili kuonyesha vile mtunzi huyu ametumia lugha katika ukuzaji wake wa maudhui kwa njia ambayo husababisha umaarufu wa nyimbo hizi. Malengo ya utafiti huu yamekuwa ni kuchanganua maudhui, kuonyesha namna matumizi ya tamathali za usemi yanavyochangia katika ukuzaji wa maudhui pamoja na kubainisha jinsi uteuzi wa kisarufi unavyodhihirika katika nyimbo za injili za Rose Muhando. Utafiti huu umeongozwa na nadharia mbili ambazo ni Uhakiki wa Kimtindo pamoja na Uadilifu. Uhakiki wa Kimtindo ni nadharia pana sana na ambayo ina mitazamo miwili; mtazamo wa kifasihi na ule wa kiisimu. Kwa mujibu wa kazi hii, mtazamo wa kifasihi uliopendekezwa na Leech na Short (1981) ndio uliotumika. Wananadharia hii wanasisitiza umuhimu wa lugha katika kazi yoyote ya fasihi. Mihimili ya nadharia hii iliyotumiwa katika uchanganuzi wetu ni miwili ambayo ni kategoria za kisarufi pamoja na tamathali za usemi. Wanauadilifu wanasisitiza umuhimu wa binadamu kuacha uovu ili awe mwadilifu. Wanatilia mkazo umuhimu wa kukuza mienendo bora ya kitabia kupitia kazi ya fasihi. Utafiti huu umefanyiwa maktabani pale ambapo makala na vitabu mbalimbali vimesomwa ili kupata yaliyoandikwa kuhusu mada ya utafiti. Mbinu ya kimaksudi imetumiwa katika uteuzi wa sampuli na ukusanyaji wa data pale ambapo data imetokana na kanda za video tepetevu za nyimbo za injili za Rose Muhando. Data yenyewe imenakiliwa na kuchanganuliwa kwa misingi ya malengo na mihimili ya nadharia ya utafiti huu. Uwasilishaji wa data umefanywa kwa njia ya kimaelezo. Uwasilishaji wa utafiti umetolewa katika sura nne. Sura ya kwanza imeonyesha mada ya utafiti, malengo ya utafiti, upeo na mipaka ya utafiti, yaliyoandikwa kuhusu mada na nadharia ya utafiti. Sura ya pili imehusisha uchanganuzi wa maudhui katika nyimbo za injili za Rose Muhando. Masuala mbalimbali ya kidini na kijamii yameweza kudhihirika katika nyimbo tulizozishughulikia. Sura ya tatu imeonyesha namna ambavyo matumizi ya tamathali za usemi yanavyochangia katika ukuzaji wa maudhui ya nyimbo za injili za Rose Muhando. Ni katika sura hii pia ambapo tumebainisha jinsi ut.e-"uzi wa kisarufi unavyodhihirika katika nyimbo tulizozishughulikia. Sura ya nne. inahusisha hitimisho la kazi hii ambapo tumetoa muhtasari, matokeo, matatizo na mapendekezo ya utafiti zaidi. Utafiti huu umekusudiwa kuwa wa manufaa kwa watafiti, wasomi wa fasihi pamoja na watunzi wa nyimbo pale ambapo umetoa mchango wa matumizi ya lugha kama mtindo wa kuwasilisha maudhui ya kifasihi. Uchanganuzi wa maudhui katika nyimbo zilizoteuliwa hautafaidi tu wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali bali utakuwa wa msaada mkubwa kwa umma unaosikiliza nyimbo za injili.
Description
Educational Management Policy and Curriculum Studies, 148 p. The PL 8702 .M83 2013
Keywords
Swahili language --Grammar, Language and languages --Style
Citation