Changamoto za uchanganuzi na ufasiriwa ushairi katika shule za upili nchini Kenya
Loading...
Date
2014-10-10
Authors
Gakuo, Joseph Kariuki
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umechanganua suala la ufasiri na uelewekaji wa ushairi wa Kiswahili
miongoni mwa wanafunzi wa shule za sekondari, Kenya. Ushairi ni somo la lazima
shuleni na ambalo kwa muda mrefu sasa limewakanganya wanafunzi wa sekondari.
Ripoti za baraza la mitihani la kitaifa zimedhihirisha matokeo mabaya ya mtihani wa
Kiswahili hususan kutokana na somo la ushairi. Hali hii imewavutia wachunguzi na
watafiti wengi kujaribu kuchangia suluhisho la kudumu kwa tatizo hili. Utanzu wa
ushairi ndio mkongwe zaidi na wenye utata na mgogoro tangu jadi. Madhali hata
tamthilia au riwaya ngumu huitwa ya kishairi. Uchunguzi huu ulijikita katika mtazamo
wa nadharia za Ki-Hemenitiki na Uhistoria mpya. Utafiti ulinuia kutathmini jinsi
ukengeushi wa Ki-Hemenitiki na kitamaduni unavyochangia ugumu wa ufasiri na
uelewekaj i wa ushairi wa Kiswahili.Ili kuafikia lengo hili la udadisi, utafiti ulihusisha
tungo mbalimbali za ushairi kutoka kwa Sauti ya Dhiki (Abdilatif Abdalla), Pambo la
Lugha (Shaaban Robert), Kina cha Maisha (Said A. Mohamed). Utafiti huu ulijikita
maktabani na nyanjani. Maktabani, utafiti ulinufaika na udurusu wa vitabu, miswada,
majarida, tasnifu, makala na machapisho yaliyoangazia masuala ya nadharia, ushairi,
uchanganuzi na tafiti kuhusu ugumu wa ufasiri wa mashairi kwajumla. Nyanjani, utafiti
ulijikita katika kaunti ya Trans Nzoia na ya Mombasa. Tulitumia sampuli ya Kimakusudi
iliyohusisha wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne. Jumla ya wanafunzi kumi
waliteuliwa kutoka katika shule nne za kila kaunti. Shule hizo zilikuwa za kategoria tatu:
Kitaifa, Kimkoa na Kiwilaya. Suala la kijinsia lilizingatiwa huku uteuzi wa sampuli
ukiegemezwa kwa malengo ya utafiti, mipaka ya utafiti na nadharia za utafiti. Tulitumia
hojaji kwa wanafunzi na walimu kutathmini mielekeo, kiwango cha uchanganuzi na
ufasiri, pamoja na mbinu na hali nzima ya ufunzaji na ujifunzaji wa mashairi na ushairi
shuleni. Tathmini hii iliegemezwa kwa vigezo vya ufasiri mwafaka wa Ki-Hemenitiki
ambavyo ni ukubalifu, uwiano, ufaafu na mshikamano. Pia, tulitumia kazi mradi kwa
wanafunzi hao kwa makusudi mawili: Tathmini ya umilisi kimsingi wa ushairi miongoni
mwao na kutathmini uwezo wao wa ufasiri mashairi. Data iliyoibuliwa ilichanganuliwa
kwa kutumia mbinu ya taraklishi ya uchanganuzi wa tarakimu sayansi za jamii. Matokeo
yalidhihirishwa kwa viwango vya kiasilimia na kuwasilishwa kwa maelezo na ufafanuzi
kwa takwimu majedwali na michoro duara. Utafiti umebaini kuwa ukengeushi wa Ki-
Hemenitiki na kitamaduni ndio sababu kuu ya ufasiri na uhakiki mbaya wa ushairi
miongoni mwa wanafunzi wa Sekondari Kenya. Utafiti umeweka bayana changamoto
nyingi zinazokumba somo la ushairi ikiwa ni pamoja na mielekeo hasi miongoni mwa
50% ya wanafunzi hao, uhuru wa kupindukia wa kukabili somo la ushairi kwa walimu,
matatizo ya lugha ya Kilahaja na Kikae, utahini wa kuyumbayumba, ukosefu wa
mwongozo wa kufundishia kwa walimu, ukosefu wa vitabu teule na cha kiada cha ushairi
na kwa jumla, ukosefu wa umilisi wa ushairi kwa wanafunzi miongoni mwa mengine.
Utafiti huu umetoa mchango mufti katika taaluma ya ushairi wa Kiswahili hususan
kuelewa jinsi ukengeushi wa Ki-Hemenitiki na kitamaduni unavyochangia ugumu wa
ufasiri na uelewekaji wa ushairi. Hili limechangia katika kusuluhisha suala la ugumu wa
ushairi miongoni mwa wanafunzi wa sekondari kwa kupendekeza jinsi viwango vya
ukengeushi katika ufasiri vinavyoweza kuzibwa.