Taswira za Ulemavu Kama Mtindo Katika Riwaya Teule za Said Ahmed Mohamed na Euphrase Kezilahabi

Loading...
Thumbnail Image
Date
2019
Authors
Mutugu, Beth Njeri
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Lengo la utafiti huu lilikuwa kuchunguza matumizi ya taswira za ulemavu kama mtindo wa kuwasilisha maudhui katika riwaya teule za Said Ahmed Mohamed na Euphrase Kezilahabi. Riwaya hizi ni: Dunia Mti Mkavu (1980), Utengano (1980), Tata zaAsumini (1990);za Said Ahmed Mohamed na Kichwamaji (1974), Dunia Uwanjawa Fujo (1975) na Rosa Mistika (1976) zilizoandikwa na Euphrase Kezilahabi. Kwa kuwa matumizi ya ulemavu kama mtindo hayajachanganuliwa katika utanzu wariwaya ya Kiswahili, utafiti huu ulinuia kuliziba pengo hili. Taswira za ulemavu zilizozingatiwa ni za ulemavu wa akili, ulemavu wa tabia na ulemavu wa viungo. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya mtindo na nadharia ya semiotiki. Nadharia ya mtindo ilimwezesha mtafiti kutambua taswira za ulemavu zilizotumika katika riwaya teule. Nadharia ya semiotiki inajikita kwenye mtazamo kuwa kiashiria kinaweza kuzua maana tofauti kulingana na muktadha wa matumizi yake. Kwa hivyo, nadharia hii iliuongoza utafiti huu katika kutambua maudhui yaliyowasilishwa kupitia kwa aina mbalimbali za ulemavu. Utafiti huu ulijikita kwenye misingi kwamba ulemavu unapotumiwa katika kazi ya fasihi, huwa ni kwa lengo mahsusi ambalo ni kuwasilisha maudhui fulani kwa njia ya kipekee. Data ilikusanywa kwa kusoma na kuzichambua riwaya teule kwa kuzingatia wahusika wenye ulemavu na jinsi walivyotumiwa kama mtindo. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa kutumia mbinu ya kimaelezo. Utafiti huu umebainisha kuwa taswira za ulemavu wa akili, ulemavu wa tabia na ulemavu wa viungo zimetumika na Said Ahmed Mohamed na Euphrase Kezilahabi kama mtindo wa kuwasilisha maudhui mbalimbali kwa njia ya kipekee. Matumizi ya mtindo huu yameiathiri hadhira lengwa ili itafakari zaidi kuhusu maswala ambayo hayajitokezi waziwazi. Maudhui yanayojitokeza ni ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Ingawa jumbe zinazowasilishwa ni za kawaida zinabeba uzito zaidi na kuiathiri hadhira zaidi zinapopitishwa kwa kutumia taswira za ulemavu. Aidha, waandishi wanafanikiwa katika lengo lao la kupitisha ujumbe wao kwa namna ya kipekee. Kwa hivyo, utafiti huuunadhihirisha kuwa mwandishi anapotumia taswira za ulemavu katika kazi yake, anafanya hivyo kwa lengo la kuwasilisha ujumbe mahsusi. Utafiti huu unatoa mapendekezo kuwa tafiti zaidi zifanywe ili kuchunguza matumizi ya ulemavu kama mtindo katika tanzu zingine za fasihi na kazi zingine zilizoandikwa na waandishi wengine wa fasihi ya Kiswahili. Aidha, inapendekezwa kuwa aina zingine za ulemavu ambazo hazijashughulikiwa katika utafiti huu zichunguzwe kwa kuzingatia matumizi yake kama mtindo. Utafiti huu utawafaidi waandishi, wahakiki, walimu na wanafunzi wa fasihi ya Kiswahili kwa kuwa unaangazia mtazamo mpya kuhusu matumizi ya ulemavu kama mtindo katika fasihi.
Description
Tasnifu Hii Imewasilishwa katika Idara ya Kiswahili, Shule ya Fani na Sayansi za Kijamii ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa Ajili ya Kutimiza Mahitaji ya Shahada ya Uzamifu, Novemba 2019
Keywords
Citation