Athari za kiswahili na kikuyu kwa uthabiti wa kishona nchini kenya:mtazamo wa kiisimujamii
Loading...
Date
2024-10
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulilenga kuchunguza athari za Kiswahili na Kikuyu kwa uthabiti wa Kiisimujamii wa Kishona nchini Kenya. Shona ni kabila mojawapo la Wabantu ambao asili yao ni nchini Zimbabwe na walifika nchini Kenya zaidi ya miaka sitini iliyopita kama wamishenari. Wameishi nchini Kenya kwa miaka hiyo yote bila utambulisho hadi mwaka wa 2020 ambapo walipewa uraia wa kuwa Wakenya. Kufikia sasa, Washona wametagusana na jamiilugha mbalimbali hapa nchini katika Kaunti ya Kiambu inayojulikana kwa wingilugha. Mtagusano lugha unapotokea, lugha husika huathirika kwa viwango mbalimbali: kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki na hata kiisimujamii. Hivyo katika kuchunguza athari hizi, malengo yafuatayo yaliongoza utafiti huu: Kuchunguza athari za mtagusano wa Kiswahili na Kikuyu kwa Kishona, kuhakiki sababu zinazopelekea Washona kutumia Kiswahili na Kikuyu katika maeneo yao ya kijamii, kudhihirisha mielekeo yao katika matumizi ya Kiswahili na Kikuyu na kubainisha iwapo Washona wamefaulu kudumisha lugha yao asilia nchini Kenya au la. Nadharia ya Uthabiti wa Kiisimujamii wa lugha iliyoasisiwa na Giles, Bourhis na Taylor (1977) na kuendelezwa na Landweer (2000) na nadharia ya Uzalishaji Kijamii ya Bourdieu (1977), zilitumika katika kuchanganua data ya utafiti. Utafiti huu ulihusisha mawanda mawili ambayo ni utafiti wa maktabani na wa nyanjani. Utafiti wa maktabani ulihusisha kudurusu miswada, vitabu, machapisho na majarida yanayoangazia uthabiti wa kiisimujamii wa lugha, nadharia za uthabiti na udumishaji wa lugha pamoja na mbinu za utafiti. Kabla ya utafiti wa nyanjani, utafiti awali ulifanyika ili kutathmini ubora wa vifaa vya ukusanyaji data. Utafiti wa nyanjani ulifanyika katika makazi ya wanajamiilugha wa Kishona ili kupata data ya moja kwa moja iliyojibu maswali ya utafiti. Jumuiya ya utafiti ilikuwa kabila la Washona wanaoishi katika mitaa mitano ya kaunti ya Kiambu. Sampuli ya utafiti huu iliteuliwa kimaksudi na kwa njia elekezi ili kumpa mtafiti uhuru wa kutathmini na kuchagua wahojiwa ambao walimpa data inayofaa kutimiza malengo ya utafiti. Mbinu zilizotumiwa katika ukusanyaji data ni pamoja na mahojiano, utazamaji au uchunzaji, mijadala ya vikundi vidogo vidogo na maswali mepesi yaliyoandaliwa awali. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa kutumia mbinu changamano. Matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo, takwimu na asilimia huku yakiongozwa na nadharia mbili za utafiti. Kufuatia juhudi za UNESCO za kudumisha lugha asilia, utafiti huu utakuwa wa manufaa kwa taifa la Kenya na mataifa mengine kwa kuwa umeongezea data muhimu katika kuhifadhi utamaduni wa Washona na mielekeo ya udumishaji kwa lugha za kabila mbalimbali.
Description
Tasnifu hii imewasilishwa kwa idara ya kiswahili ili kutosheleza mahitaji ya shahada ya uzamifu katika chuo kikuu cha kenyatta, Oktoba 2024
Wasimamizi
Dkt. Stephen Njihia Kamau
Dkt. Boniface Ngugi