Matumizi ya Mbinu Inayotegemea Shughuli za Mwanafunzi katika Ufundishaji wa Riwaya kwa Shule za Upili katika Kaunti ya Makueni, Kenya

Loading...
Thumbnail Image
Date
2021
Authors
Koka, Juliens Mumangi
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Mbinu zinazotumiwa katika ufundishaji huchangia pakubwa uelewa wa mwanafunzi na kile kinachofundishwa. Utafiti huu ulidhamiria kuchunguza namna mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi inavyotumiwa katika kufundishia riwaya ya Kiswahili. Mbinu zinazotumiwa katika ufundishaji darasani huathiri pakubwa kiwango cha uelewa wa wanafunzi wa kile kinachofundishwa. Utafiti huu ulidhamiria kutimiza madhumuni yafuatayo: kubainisha mbinu zinazotumiwa kufundishia riwaya, kuchunguza ni kwa kiwango kipi walimu wa fasihi wanatumia mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi, kuchunguza athari za mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi kwa utendaji wa wanafunzi, kubainisha mitazamo ya walimu kuhusu mbinu inayotegemea shughuli za wanafunzi na kutambua changamoto za walimu wanapotumia mbinu husika. Utafiti huu ulifanyika katika kaunti ndogo ya Mukaa, kaunti ya Makueni. Utafiti uliongozwa na nadharia ya ubunaji. Uchanganuzi wa data ulifuata muundo wa kimaelezo. Mtafiti alitumia uteuzi makusudi kuteua shule katika viwango vya kitaifa, kaunti na kaunti ndogo. Idadi ya watafitiwa katika utafiti huu ilihusisha sampuli lengwa na sampuli mahususi. Sampuli lengwa ilikuwa shule 43, walimu 60 na wanafunzi 2850. Uteuzi makusudi ulitumika tena kuteua madarasa ya wanafunzi na walimu wao. Nayo idadi mahususi ilikuwa shule 6, walimu 12 na wanafunzi 540. Data ilikusanywa kutumia: hojaji, mahojiano uchunzaji darasani na mtihani wa mwanzoni na mwishoni mwa utafiti. Data ilichanganuliwa kwa muundo wa kimaelezo, kithamani na kiidadi. Data hiyo iliwasilishwa kwa kutumia maelezo, majedwali na grafu. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa walimu wengi hutumia mbinu za kawaida na ambazo walizizoea mno katika ufundishaji wa riwaya kama vile mbinu ya mhadhara na ya masaili. Aidha mbinu zinazowashirikisha zaidi wanafunzi ziliepukwa sana na walimu. Mbinu inayotegemea shughuli za wanafunzi haikutumiwa sana na walimu. Ilibainika wazi kuwa wanafunzi wanapofundishwa kwa mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi huelewa vyema kuliko vile wanavyoelewa wakifundishwa kwa mbinu za kawaida. Walimu wengi walikuwa na mtazamo hasi kuhusiana na mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi. Pia walimu walikabiliwa na changamoto kadha wakati wa matumizi ya mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi katika ufundishaji wao ikiwepo changamoto ya ukosefu wa muda wa kutosha na kazi nyingi kwa walimu wanapotekeleza mbinu hiyo. Utafiti huu utakuwa wa umuhimu mkubwa kwa makundi mbalimbali ya watu katika eneo la utafiti yakiwemo yafuatayo: walimu wa fasihi katika shule za upili, maafisa wa kukadiria ubora wa viwango vya elimu, wanafunzi wa somo la fasihi, taasisi ya kukuza mtaala ya Kenya na mwisho kabisa kwa watafiti wengine ambao wangetaka kutafiti kuhusu ufundishaji wa riwaya. Kwa ujumla utafiti huu utaboresha ufundishaji wa riwaya katika shule za upili. Utafiti huu ulipendekeza walimu wafanyiwe mafunzo zaidi ili waweze kutumia mbinu inayotegemea shughuli za mwanafunzi katika ufundishaji wao wa riwaya na kukabiliana na changamoto zake. Mapendekezo zaidi yalifanywa ili kuweza kuimarisha ufundishaji wa riwaya.
Description
Tasnifu hii Inawasilishwa ili Kutosheleza baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Idara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Elimu, Kitivo kha Elimu, Chuo Kikuu Cha Kenyatta, Oktoba 2021
Keywords
Matumizi, Mbinu Inayotegemea, Shughuli za Mwanafunzi, Ufundishaji wa Riwaya, Shule za Upili, Kaunti ya Makueni, Kenya
Citation