PHD-Department of Kiswahili & African Languages
Permanent URI for this community
Browse
Browsing PHD-Department of Kiswahili & African Languages by Subject "Ken Walibora"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Umahuluti wa Riwaya ya Kiswahili: Uchunguzi wa Riwaya Teule za Ken Walibora na Katama Mkangi(Kenyatta University, 2021) Sululu, Simiyu Benson; Richard M. Wafula; Joseph N. MaitariaUtafiti huu ulishughulikia umahuluti wa riwaya ya Kiswahili kupitia uchunguzi wa riwaya teule za Ken Walibora na Katama Mkangi. Riwaya zilizozingatiwa katika utafiti huu ni: Kufa Kuzikana (2003) na Ndoto ya Almasi (2006) za Ken Walibora na Mafuta (1984) na Walenisi (1995) za Katama Mkangi. Utafiti huu ulichochewa na sababu kwamba riwaya ya Kiswahili ni mojawapo ya tanzu za fasihi ambapo waandishi wake wameibuka kutoka jamii tofauti za Kiafrika. Kwa hivyo, utafiti huu ulinuia kudhihirisha namna tamaduni na fasihi simulizi za watunzi wa Kiafrika wa riwaya ya Kiswahili, wasiokuwa Waswahili wa kuzaliwa, zimeanza kuchangia riwaya ya Kiswahili na kuifanya kuwa ya kimahuluti. Suala hili halijafanyiwa utafiti wa kina. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kubainisha muktadha ulioambatana na mazingira wanamotoka watunzi teule na kufafanua namna tanzu za kimaigizo, kinathari na kishairi za fasihi simulizi za watunzi hawa zilichangia umahuluti wa riwaya zao teule. Nadharia ya Umahuluti wa Utamaduni na nadharia ya Mwendelezo wa Kikrioli ndizo zilizotumiwa katika utafiti huu. Nadharia ya Umahuluti wa Utamaduni ilifaa kwa kumwezesha mtafiti kuchanganua na kufasiri namna umahuluti hutokea katika miktadha ya utambulisho wa asili na tamaduni za waandishi teule wa riwaya ya Kiswahili. Nadharia ya Mwendelezo wa Kikrioli ilimfaa mtafiti kuhakiki na kuchimbua jinsi umahuluti hutokea katika kiwango cha kiisimu ambapo watunzi teule huandika kazi zao katika lugha ya Kiswahili huku wakitumia misimbo ya lugha zao za Lubukusu na Kiribe. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani na nyanjani. Maktabani, mtafiti alisoma kwa kina riwaya teule nne na kudondoa mifano ya matumizi ya tanzu za fasihi kwa minajili ya kuzilinganisha na zile za fasihi simulizi za jamii za watunzi ili kubainisha umahuluti. Aidha, mtafiti alisoma vyanzo mbalimbali na kunukuu data ya sekondari iliyojumuisha maoni ya wataalam wa masuala ya fasihi kuhusu uhusiano baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi na jinsi mwingiliano wa aina hizi za fasihi huchangia kuzuka kwa utanzu wa kimahuluti. Nyanjani mtafiti alitumia hojaji, maswali ya mahojiano na uchunzaji mahuluti ili kupata data ya msingi kuhusu tanzu za fasihi simulizi za jamii wanakotoka Ken Walibora na Katama Mkangi. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kwamba Ken Walibora na Katama Mkangi walizaliwa na kulelewa katika mazingira yaliyosheheni miktadha maalum ya fasihi simulizi. Uchanganuzi ulionyesha kwamba Ken Walibora na Katama Mkangi wametumia tanzu za kimaigizo, kinathari na kishairi kutoka fasihi simulizi za jamii zao kuchangia muundo, usawiri wa maudhui, ubainishaji wa sifa za wahusika pamoja na mtindo katika riwaya zao teule za Kiswahili na hivyo kuzifanya riwaya hizo kuwa za kimahuluti. Utafiti huu umechangia katika kufahamu utepetepe na unyumbufu wa riwaya ya Kiswahili kama utanzu unaomeza tanzu zingine na kukubali mifumo anuwai ya lugha huku ukihifadhi umbo lake kama riwaya ya Kiswahili. Vilevile, utafiti huu umechangia katika kufufua nafasi ya mtunzi katika ufasili wa kazi yake kwa kuzingatia muktadha wa maisha yake. Aidha, utafiti huu umedhihirisha maendeleo ya lugha ya Kiswahili kutoka lugha iliyonasibishwa na kabila fulani hadi nafasi ambapo lugha hii sasa imedhihirisha sifa za kitaifa na kimataifa kupitia watunzi anuwai wanaotumia lugha hii na hivyo kuifanya kuwa ya kimahuluti.