PHD-Department of Kiswahili & African Languages
Permanent URI for this community
Browse
Browsing PHD-Department of Kiswahili & African Languages by Subject "Itikadi"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Itikadi za Kiuana Katika Methali za Kinyankole na Kiswahili(Kenyatta University, 2023) Lubuuka, Yunusu; Catherine Ndung'o; Jesse Joseph MurithiUtafiti huu umechunguza itikadi za kiuana katika methali za Kinyankole na Kiswahili. Utafiti umedhamiria kubainisha itikadi za kiuana na vile zinavyoendeleza mahusiano ya kiuana kwa ukubalifu na ushawishi kati ya wanaume na wanawake. Itikadi kama imani za watu zina nguvu za kuwashawishi na kuwafanya wakubali nafasi zao na majukumu kwa misingi ya maumbile yao. Fikira na mielekeo katika mahusiano yao ya kawaida huganda akilini mwao na kuchukulia mambo kuwa ya kawaida. Imani hizi kuhusu mahusiano ya kiuana kati ya wanaume na wanawake zinaendelezwa kwa ukubalifu na ushawishi ulio na msingi katika utamaduni wa jamii zinazotawaliwa kwa mfumodume. Jambo hili limeafikiwa kwa kuchunguza mahusiano ya kiuana yanayodhihirishwa na itikadi za kiuana katika methali za Kinyankole na Kiswahili. Aidha, utafiti umehakiki methali zinavyoibua ukinzani wa itikadi za kiuana na athari zake kuhusu usawa wa kiuana katika methali za Kinyankole na Kiswahili. Kadri ajuavyo mtafiti, uhakiki na utafiti wa kina umekuwa haujafanywa kubainisha itikadi za kiuana zinavyoendeleza mahusiano ya kiuana kwa ukubalifu na ushawishi kati ya wanaume na wanawake. Vitabu vinne vya methali za Kinyankole na Kiswahili vimeteuliwa kuhusu itikadi za uana kwa njia ya kusudio. Vitabu hivi ni; Enfumu z’Omurunyankore Rukiga (Saite: 1989), Kamusi ya methali za Kiswahili (King’ei na Ndalu: 1989), Kamusi ya Methali (Wamitila: 2001) na Dafina Hazina ya Kiswahili (Al Haj Al Habsy, 2012). Data ambayo imekusanywa inahusu methali ambazo zinawasilisha itikadi za kiuana katika jamii ya Wanyankole na Waswahili. Nadharia za Itikadi Gramsci (1971), Ufeministi wa Kiafrika ya Steady (1981) na Udenguzi ya Derrida (1960) zimetumika. Nadharia ya Itikadi imetufaa katika kuwasilisha na kuchanganua itikadi mbalimbali zilizomo katika methali za Kinyankole na Kiswahili pamoja na kutathmini jinsi itikadi hizo zinazoendeleza mahusiano ya kiuana kwa ukubalifu. Nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika kimsingi inalenga kuendeleza usawa wa kiuana bila ubaguzi wa binadamu katika misingi ya maumbile yao kijinsia pamoja na kuchunguza tofauti za kiuana zilizopo, na ambazo zinajikita katika amali za kijamii, kisiasa na kitamaduni. Mtazamo huu wa kinadharia umetumiwa kuelewa bayana itikadi za kiuana, mahusiano yake kimajukumu na jinsi itikadi hizo zinavyoathiri usawa wa kiuana kupitia methali za Kinyankole na Kiswahili.Vilevile, tumetumia nadharia ya Udenguzi kama inavyoendelezwa na Abrams na Harpham (2014). Nadharia hii imelenga kuhakiki methali ili kubainisha ukinzani wa itikadi za kiuana na athari zake kwa usawa wa kiuana. Nadharia hii imetuwezesha kufafanua methali kwa kina kwa kuibua fasili mbalimbali ambazo zimetubainishia itikadi zinazokinzana. Mbinu za utafiti ambazo zimetumika ni za maktabani na nyanjani. Maktabani, data imekusanywa kutokana na uchambuzi wa vitabu vya methali kutoka kwenye maktaba na makavazi ya Ankole, maktaba ya umma iliyoko Mombasa, maktaba ya ngome ya Fort Jesus na maktaba ya Lamu Fort. Data kutoka nyanjani inahusu maoni ya wasailiwa juu ya itikadi za kiuana katika methali kwa muktadha wa tamaduni za jamii za Wanyankole na Waswahili pamoja na methali. Utafiti umetumia mwongozo wa maswali na vinasa sauti kupata data pamoja majadiliano na wahojiwa. Wilaya za Kiruhura, Sheema nchini Uganda na miji ya pwani ya Mombasa, Lamu na Zanzibar zimehusishwa katika utafiti huu. Sampuli ya kusudio imetumiwa katika kutambua na kuwahoji wasailiwa ambao ni wanaume na wanawake wataalamu pamoja na wasomi wenye umri wa makamo. Data imechanganuliwa kwa mtindo wa kimaelezo na kuwasilishwa kwa mujibu wa malengo ya utafiti kwa kuongozwa na nadharia lengwa. Hatimaye itikadi za kiuana zimebainishwa na vile zinaendeleza mahusiano ya kiuana kwa ukubalifu. Aidha, methali za Kinyankole na Kiswahili zimeonyeshwa namna zinavyoibua ukinzani wa itikadi za kiuana na athari zake kuhusu usawa wa kiuna.