Browsing by Author "Munyao, Carolyne Nzilani"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Tathmini ya Uainishaji wa Tanzu na Vijitanzu vya Fasihi Simulizi katika Vitabu Vilivyoidhinishwa: Kaunti ya Makueni(Kenyatta University, 2025-10) Munyao, Carolyne NzilaniUtafiti huu unahusu tathmini ya uainishaji wa tanzu na vijitanzu vya fasihi simulizi katika vitabu vilivyoteuliwa kufunza fasihi simulizi ya Kiswahili kwa walimu na wanafunzi katika Shule za Upili Kenya, Kaunti ya Makueni. Utafiti ulilenga kuonyesha ukinzano wa idadi ya tanzu na vijitanzu na matatizo yanayokumba wanafunzi na walimu katika uainishaji wa fasihi simulizi. Masuala matatu yalilengwa katika utafiti huu: kubainisha tofauti katika uainishaji wa tanzu na vijitanzu vya fasihi simulizi katika vitabu vilivyoidhinishwa, kubainisha vigezo vilivyotumiwa na kupendekeza suluhisho kwa utata unaotokana na tofauti hizi za uainishaji. Nadharia mbili zilitumiwa:ya Tanzu na ya Ujifunzaji na Upokeaji wa Lugha ya Pili (Second Language Learning and Acquisition) iliyoasisiwa na Krashen (1982) ambapo haipothesia ya mchakato (Input hypothesis) zilitumiwa kufanikisha malengo ya utafiti huu. Haipothesia hii ilihusu sheria katika upokezi wa lugha, kusonga kutoka kwa dhana rahisi hadi ngumu na uelewa wa maarifa kutoka (i+1) ambapo i ni maarifa yaliyopo tayari na 1 ni maarifa yanayopatikana baadaye kupitia ujifunzaji. Nadharia ya Tanzu ilijikita kwa maswali je, tanzu zipo? Je, kuna idadi mahsusi ya tanzu? na Je, tanzu zinajisimamia au zinaingiliana? Nadharia hii ililenga uainishaji wa tanzu na vigezo vya uainishaji. Uteuzi wa kimakusudi ulitumiwa kuteua vitabu vilivyoidhinishwa na taasisi ya kukuza mitaala vya kufundishia fasihi simulizi kwa shule za upili, vitabu hivi viliwapa watafiti data ya kimsingi (maktabani) ilhali data endelezi (nyanjani) ilitokana na wanafunzi na walimu. Shule nne za upili ziliteuliwa ambapo wanafunzi ishirini wa kidato cha nne walihojiwa. Aidha, walimu wawili wa Kiswahili katika kila shule waliteuliwa na kuhojiwa. Muundo wa utafiti huu ni wa kimaelezo. Data iliyopatikana ilichanganuliwa kwa mtindo wa kimaelezo na kuwasilishwa kwa maelezo fafanuzi na majedwali. Matokeo ya utafiti huu yalibainisha kuwa vitabu tofauti vilivyoidhinishwa kufundishia fasihi simulizi kwa shule za upili vilikuwa na uainishaji unaotofautiana wa tanzu na vijitanzu vya fasihi simulizi. Baadhi ya vitabu vina tanzu nne, vingine tano na vingine sita. Pamoja na hayo, utafiti ulibaini kuwa uainishaji wa tanzu na vijitanzu vya fasihi simulizi unategemea vigezo na misingi mbalimbali inayofuatwa na wataalamu katika kuandika matini za fasihi simulizi kama vile; muundo, maudhui, wakati, mtindo, wahusika na kadhalika. Ilibainika kuwa, ni kwa sababu hii kunatokea utata katika vitabu vilivyoidhinishwa. Kwa mujibu wa nadharia ya Ujifunzaji na Upokeaji wa Lugha ya Pili, iwapo mada zitawasilishwa kwenye vifaa kwa njia isiyo wazi basi kutakuwa na changamoto kwa wasomaji. Aidha, kupitia hojaji, wasailiwa walikiri kuwa kuna utata katika ufundishaji na usomaji wa fasihi simulizi kutokana na hali hii. Hivyo basi, mtafiti alipendekeza kuwa, mada za fasihi simulizi zinastahili kuratibiwa upya ili ziwafae wanafunzi na walimu katika shule za upili. Utafiti huu ni wa manufaa kwa watafiti, wahakiki, waandishi wa vitabu vya fasihi simulizi, walimu na wanafunzi wa Shule za Upili na waratibu wa mitaala.