Browsing by Author "Munguti, Catherine Ndinda"
Now showing 1 - 1 of 1
Results Per Page
Sort Options
Item Usawiri wa Wahusika Vimada Katika Riwaya Teule za John Habwe: Mfano Kutoka kwa Paradiso (2005), Cheche za Moto (2008) na Safari ya Lamu (2011)(Kenyatta University, 2025-06) Munguti, Catherine Ndinda; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu umechunguza usawiri wa vimada katika riwaya teule za John Habwe. Riwaya zilizoteuliwa katika utafiti huu ni zifuatazo: Paradiso (2005), Cheche za Moto (2008) na Safari ya Lamu (2011). Riwaya hizi ziliteuliwa kutokana na motifu ya wahusika vimada wanaobainika wakiwemo Sakina, Fatuma na Maimuna mtawalia. Uchunguzi wa usawiri wa vimada ulikuwa muhimu kwa sababu ni suala ibuka katika jamii ya kisasa. John Habwe ameziandika riwaya zenye kuwaibua wahusika vimada wanaoishi na wanaume nje ya misingi ya ndoa. Tafiti mbalimbali zimefanywa kuhusu usawiri wa wahusika katika utanzu wa riwaya ya Kiswahili. Baadhi ya tafiti hizi ni pamoja na Muindi (1990), Saro (2017), Mavisi (2019) na Kanwa (2022). Tafiti hizi zimeeleza usawiri wa wahusika wa wanawake kwa jumla katika riwaya. Hata hivyo, hazijaweza kufafanua usawiri wa wahusika vimada jambo ambalo limefanywa na utafiti huu. Malengo ya utafiti huu ni: kufafanua usawiri wa wahusika vimada katika riwaya teule, kubaini vichocheo kwa wahusika kuwa vimada na kuchanganua athari za hali ya maisha ya wahusika vimada katika riwaya teule. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uhalisia. Nadharia ya Uhalisia iliasisiwa na Georg Lukacs (1938). Nadharia hii hueleza ukweli kama ulivyo katika jamii. Mihimili ya nadharia ya uhalisia iliufaa utafiti huu kwa kuonyesha kuwa John Habwe anawachora wahusika vimada kama wanavyojitokeza katika jamii. Data ya kimsingi ilitoka kwenye riwaya teule. Riwaya teule zilisomwa ili kupata kauli na matendo ya wahusika vimada. Utafiti huu ni wa kimaelezo ambapo kila lengo lilichanganuliwa katika sura yake mahususi kwa kuihusisha mihimili ya nadharia ya Uhalisia. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani ambapo vitabu, tasnifu na majarida yalisomwa pamoja na kusakura mitandao ili kupata tafiti zilizokuwa za punde zaidi kote ulimwenguni. Utafiti umegundua kuwa wahusika vimada wamesawiriwa kwa hali chanya katika mahusiano yao na wahusika wengine katika riwaya teule. Isitoshe, utafiti umebaini kuwa wahusika vimada katika riwaya teule wameathiri maisha ya wahusika wengine kwa namna chanya na kuishia kuboresha hali ya maisha ya wahusika wanaokaa nao kinyumba. Utafiti huu unatarajiwa kutoa mchango katika uhakiki wa utanzu wa riwaya kuhusu usawiri wa wahusika katika riwaya ya Kiswahili.