Mabadiliko ya Kihistoria katika Fonolojia ya Kiswahili: Udondoshaji wa Fonimu
Loading...
Date
2021
Authors
Kiplimo, Cheruiyot Evans
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza mabadiliko ya kihistoria ya udondoshaji wa sauti za likwidi katika maneno ya Kiswahili. Kimsingi, silabi katika lugha huchukua mfumo wa konsonanti (K) kabla ya vokali (V) na huwakilishwa kama KV (Oostendorp, 2005 & Yule, 2010). Muundo wa silabi ya KV upo katika Kiswahili. Hyman (2003b) anabaini kuwa, silabi inayokubalika katika Mame-bantu imebanwa katika miundo ya KV, KVV na V. Miundo hii ya silabi ipo katika Kiswahili na baadhi yake ni matokeo ya mabadiliko ya kihistoria ya udondoshaji wa fonimu. Fonimu /l/ na /r/ zina mazoea ya kudondoshwa katika mazingira mahususi japo ithibati hazijatolewa. Utafiti huu ulichanganua maneno arubaini yaliyokusanywa kutoka Kamusi Kuu ya Kiswahili (2015). Malengo ya utafiti ni pamoja na kudhihirisha udondoshaji wa fonimu /l/ na /r/ katika maneno ya Kiswahili, kueleza sababu zake kutokea na kubainisha athari zake katika fonolojia arudhi ya Kiswahili. Nadharia ya fonolojia zalishi ya Chomsky na Halle (1968) iliteuliwa kuongoza utafiti huu. Mbinu ya uundaji ndani na mbinu linganishi zilitumiwa kupata ithibati iliyotumiwa kuthibitisha udondoshaji huu. Kwa kutumia mbinu ya uundaji ndani, maumbo awali ya maneno ya sasa yalionyeshwa na udondoshaji uliotokea na pale ambapo ushahidi ulikosekana, mbinu linganishi ilitumika kulinganisha maneno ya Kiswahili na mengine ya mnasaba (Ekegusii, Kikuyu, Kiluhya, Kimeru, Kitaita na Kikamba). Data ya maktabani iliwekea msingi upataji wa data ya nyanjani ambayo ilikusanywa kupitia kwa maswali ya hojaji. Sampuli ya maneno iliyofaa katika utafiti huu iliteuliwa kimaksudi pamoja na walengwa watano katika lugha zilizoteuliwa. Hatua hii ilikuwa muhimu kwa sababu mtafiti aliweza kulinganisha, kulinganua na kuunda upya leksika ya Kiswahili. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo, majedwali na unukuzi wa sheria za kifonolojia. Utafiti huu ulibaini kuwa fonimu za likwidi hudondoshwa katika mazingira ya kuwepo katikati ya vokali mbili. Kando na hayo, utafiti ulionyesha kuwa fonimu za likwidi zilidondoshwa kwa sababu ya haja ya kurahisisha matamshi na utashi wa wazungumzaji. Fonimu hizi zinapodondoshwa lugha hupata miundo changamano kifonetiki na hata kwenye miundo ya silabi. Udondoshaji unapotokea katika vitenzi teule, badiliko lingine (uchopekaji) linatokea ili kuhifadhi sheria ya uziada na kuleta mfumo unaokubalika. Utafiti huu uligundua kuwa, sheria ya udondoshaji wa kihistoria wa fonimu za likwidi haina tija katika Kiswahili cha sasa kwa sababu baadhi ya maneno yana mazingira ya udondoshaji ilhali udondoshaji hautokei. Utafiti huu unaweza kuendelezwa kwa kutumia nadharia nyinginezo pamoja na data ya asili tofauti kama vile kwenye hifadhi ya maandiko. Utafiti huu ulitoa mchango katika isimu historia na fonolojia ya Kiswahili.
Description
Tasnifu hii Imewasilishwa Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Desemba, 2021
Keywords
Mabadiliko, Kihistoria, Fonolojia ya Kiswahili, Udondoshaji, Fonimu