Miima FlorenceOndigi SamsonKalabai, Sikolia Cleophas2022-08-232022-08-232022http://ir-library.ku.ac.ke/handle/123456789/24045Tasnifu hii Inawasilishwa kwa Minajili ya Kutosheleza Mahitaji ya Shahada ya Uzamifu katika Elimu ya Lugha Kitivo cha Elimu Chuo Kikuu cha Kenyatta, Juni, 2022Kusoma ni stadi ya lugha ambayo hufundishwa shuleni. Stadi hii hufundishwa kwa lengo la kuimarisha uwezo wa mwanafunzi wa kujifunza maarifa katika makala na kufaulu masomoni. Umuhimu huu unafanya kusoma kuwa stadi inayostahili kufundishwa vyema katika kila darasa. Hata hivyo, wanafunzi wengi wa shule za msingi nchini Kenya hawana uwezo wa kusoma makala ya Kiswahili ya kiwango chao cha ujifunzaji. Hali hii inachangiwa na walimu kutumia mikakati ya kawaida ambayo haiwezi kuimarisha usomaji wa wanafunzi. Walimu wanafaa kutumia mikakati ambayo ilitafitiwa na kubainika kuwa bora kwa ufunzaji wa kusoma. Somo la Kiswahili halina mikakati mingi iliyotafitiwa na kufahamika kuwa bora kwa ufunzaji wa stadi hii licha ya kudorora kwa viwango vya usomaji shuleni. Mikakati zaidi inahitajika kufanyiwa utafiti na kutumiwa shuleni ili kuimarisha usomaji wa wanafunzi. Lengo la utafiti huu lilikuwa kuchunguza athari za Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kwa wanafunzi katika kusoma Kiswahili kama lugha ya pili. Lengo hilo liliafikiwa kwa shabaha zifuatazo: kuchunguza athari za Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kwa wanafunzi katika kusoma Kiswahili kama lugha ya pili; kubaini athari za Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kwa usomaji wa wanafunzi kwa misingi ya kijinsia; kuchunguza athari za Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kwa wanafunzi katika kubaini maana ya msamiati kwenye makala ya Kiswahili; kufafanua athari za Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kwa wanafunzi katika kutambua maana ya uamala katika makala ya Kiswahili; kutambua mtazamo wa wanafunzi kwa Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari katika ufunzaji wa kusoma Kiswahili kama lugha ya pili; kueleza matatizo yanayotokana na matumizi ya Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari katika ufunzaji na ujifunzaji wa kusoma Kiswahili kama lugha ya pili. Utafiti huu ulizingatia muundo wa kijarabati mahuluti na kuongozwa na nadharia ya tamaduni za kijamii na ujifunzaji wa kijamii. Uliwashirikisha wanafunzi 72 wa darasa la nne na walimu 4 waliokuwa wakiwafundisha Kiswahili. Walimu na wanafunzi waliteuliwa kwa kutumia mbinu ya kimaksudi, utabakishaji na nasibu sahili. Data ilikusanywa kwa hojaji, mahojiano ambayo hakuratibiwa, uchunzaji na mijarabu miwili na ikachanganuliwa kwa ANOVA. Matokeo yalionyesha kuwa mkakati wa Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari ulikuwa na athari chanya kwa wanafunzi katika kusoma Kiswahili kuliko mikakati ya kawaida. Mkakati huu pia uliweza kuimarisha uwezo wa wanafunzi wa kubaini maana ya uamala kuliko mikakati ya kawaida. Isitoshe, wanafunzi walikuwa na mtazamo chanya kwa mkakati wa Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari walipoutumia kujifunza kusoma. Zaidi ya hayo. mkakati wa Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari haukupendelea jinsia yoyote katika kusoma Kiswahili. Isitoshe, haikutofautiana na mikakati ya kawaida katika kuathiri uwezo wa wanafunzi wa kutambua maana ya msamiati. Kutokana na matokeo hayo, utafiti huu ulipendekeza kuwa walimu watumie Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kufundisha kusoma Kiswahili kama lugha ya pili. Walimu pia watumie Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kufundisha kusoma wakati mikakati mingine inaposhindwa kuafikia shabaha za somo hili. Mwisho, walimu watumie Shughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari kufundisha stadi zingine za lugha kama vile kusikiza na kuandika.enShughuli ElekeziKusomaKutafakari:Athari kwa UsomajiWanafunziShule za MsingiKaunti ya BungomaKenyaShughuli Elekezi ya Kusoma na Kutafakari: Athari kwa Usomaji wa Wanafunzi wa Shule za Msingi katika Kaunti ya Bungoma, KenyaThesis