Rais, Abdu Salim2023-08-112023-08-112023http://ir-library.ku.ac.ke/handle/123456789/26788Tasnifu hii imetolewa kwa shule ya sheria, sanaa na sayansi za jamii ili kutosheleza mahitaji ya shahada ya uzamifu ya kiswahili katika chuo kikuu cha Kenyatta Mei, 2023Utafiti huu umejitenga na tafiti zilizopo kwa kuwa, ulitathmini maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda katika muongo wa pili wa karne ya ishirini na moja, kwa kuchunguza uhusiano katika ukuaji na ueneaji wa matumizi yake. Watafiti wengi kama vile Mbaabu (1991) na Mlacha (1995) waliandika mengi kuhusu historia ya maendeleo ya Kiswahili, usanifishaji na sera za lugha kabla na baada ya mwaka 1928. Hata hivyo, kufikia wakati wa kukamilisha utafiti huu, hakukuwa na utafiti wa kina uliofanywa kutathmini viwango vya ukuaji na ueneaji wa matumizi ya Kiswahili nchini Uganda tangu 2011, licha ya Kiswahili kuendelea kukabiliana na changamoto tofauti. Kwa hivyo, mtafiti alikusudia kuziba pengo hilo. Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa, kutathmini maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda. Malengo mahsusi yalikuwa; kuchunguza ukuaji wa matumizi ya Kiswahili, kuchambua ueneaji wa matumizi ya Kiswahili, kubainisha uhusiano baina ya ukuaji na ueneaji wa matumizi ya Kiswahili na kutambua vihamasisho vilivyochangia maendeleo yake nchini Uganda. Upeo wa utafiti huu ulijikita katika asasi za kijamii k.v; biashara, elimu, siasa, dini na burudani. Utafiti huu ulifanyika Kampala nchini Uganda. Uamilifu wa Kiswahili ulibainishwa na nadharia ya Uamilifu iliyoasisiwa na wanasosholojia Auguste Comte (1787-1857), Herbert Spencer (1830-1903), Vilfredo (1848-1917) na Emile Durkheim (18571917) na kundelezwa na Mesthrie na wengine (2004). Nadharia hiyo iliwasilisha wazo kwamba, uamilifu ni lile jukumu ambalo hutekelezwa na fani katika jamii fulani. Nadharia hiyo ilitumiwa kutathmini dhima ya Kiswahili nchini Uganda. Pamoja na nadharia hiyo, nadharia ya Utegemezi (Ferraro, 2008) ilitumika. Utaratibu wa utafiti ulihusisha miundo ya kithamano na kiwingiidadi iliyotumika kwa kuzingatia mkabala wa mwimarishopembetatu katika ukusanyaji, uchanganuzi na uwasilishaji data. Data ilielezwa kwa kutumia asilimia za maratokezi kutokana na takwimu za matokeo ya maoni ya wahojiwa. Data ya utafiti huu ilikuwa unukuzi kutokana na nyaraka za hifadhi za maandishi asili ya asasi mbalimbali, maoni ya wataalamu na matokeo ya wahojiwa wa hojaji zilizochanganuliwa kwa kutumia programu ya SPSS. Sampuli ya wahojiwa waliojaza hojaji ilitokana na orodha ya walimu kutokana na jukwaa la Chakitau wasiozidi mia moja wilayani Kampala na ilibainishwa kupitia kigezo cha uteuzi wa sampuli cha Krejcie na Morgan (Amin, 2005). Wahojiwa wengine wa utafiti huu walitokana na asasi mahsusi zenye uhusiano na maswala ya Kiswahili k.v; wataalamu na wakuu wa vitengo mbalimbali walioteuliwa kimaksudi kupitia mbinu ya sampuli mkufu. Matokeo ya utafiti huu yatatoa mchango maalumu katika kuongezea kanzi ya elimu ya lugha kwa maarifa mapya kuhusu maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda. Utafiti huu utapanua upeo wa tafiti za siku zijazo kuhusu maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda. Matokeo ya utafiti yatachangia swala la uteuzi wa lugha ya taifa. Vile vile, utafiti huu utasaidia kukadiria manufaa ya Kiswahili katika asasi za kijamii k.v; elimu, biashara, siasa, ulinzi, dini, mawasiliano, utangazaji na burudani (Michira na wenzake, 2014).otherkiswahiliUgandaMaendeleo ya kiswahili nchini Uganda katika karne ya ishirini na mojaThesis