Lucas, Priscah Katunge2025-02-112025-02-112024-11https://ir-library.ku.ac.ke/handle/123456789/29559Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Novemba 2024. Msimamizi Leonard ChachaUtafiti huu ulichunguza udhihirikaji wa viambajengo katizwa katika Kiswahili. Kwa kawaida lugha huwa na viambajengo vinavyofululiza ili kutoa maana inavyopasa. Mara chache, lugha itakuwa na viambajengo visivyofululiza na kati ya hivyo kuna vinavyokuwa na maana na kuna visivyokubalika. Viambajengo katizwa ni elementi za neno au kishazi ambazo hazipatikani katika usanjari mmoja kwa sababu elementi kutoka mofu au kirai kingine zimeingilia kati (Reinholtz, 1999). Hili hutokea wakati mofu kadhaa za kiambajengo kimoja zimetengwa au maneno kadhaa ya kirai kimoja yametengwa. Kulingana na Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (Massamba, 2004), mofimu ambayo inaanza halafu inaingiliwa kati na mofimu nyingine kisha inaendelea huitwa mofimu katizwa. Ifuatayo ni mifano, mmoja wa kiwango cha mofolojia na mwingine ukiwa wa kiwango cha kisintaksia. (a) Wa-me-chek-a (yakinifu) -Ha-wa-ja-chek-a (kanushi). Katika mfano huu, mofu ha- na -ja- zilirejelea ukanushaji lakini zilitengwa na kiambishi -wa- cha mtenda. (b) “Rais alizungumza, bila shaka, juu ya siasa.” Katika sentensi hii, kitenzi na kielezi chake vilitengwa na taarifa nyingine. Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo: kudhihirisha mofimu katizwa katika lugha ya Kiswahili, kuchanganua viambajengo katizwa katika kiwango cha virai na sentensi za Kiswahili na kuainisha viambajengo katizwa katika lugha ya Kiswahili. Nadharia ya Sarufi Miundo Virai Katizwa iliyozungumziwa na Harman (1963) iliongoza utafiti huu. Nadharia hii ilionesha jinsi vipashio katika kirai vilitegemeana na kuwezesha mistari ya ukingamo kuchorwa ili kuonesha vipashio vilivyoingilia kati viambajengo vinavyozungumziwa. Utafiti huu ulifanywa maktabani na pia nyanjani. Data nyingi ilikusanywa kutoka nyanjani ambapo wataalamu wa lugha ya Kiswahili walihojiwa kuhusu usahihi wa sentensi katizwa na hata kusaidia kuzalisha zingine. Mbinu ya usampulishaji wa kimaksudi ilitumika katika uteuzi wa sampuli. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa maelezo, majedwali na michoroti. Kutokana na utafiti huu, ilibainika kuwa viambajengo katizwa husababishwa na uchopekaji wa neno, tungo au mofu nyingine kabla ya kumalizika kwake. Mofimu katizwa ilibainika kujidhihirisha kupitia njia ya ukanushi na ukanushi maradufu. Utafiti huu ulibaini aina mbili kuu za virai katizwa. Sentensi katizwa ziliainishwa kulingana na dhamira, vishazi bebwa, vishazi vya masharti n.k. Tafiti zingine zinaweza kufanywa kuhusu udhihirikaji wa viambajengo katizwa katika aina nyingine ya kirai kama vile kirai kihusishi au kirai kivumishi katika lugha ya Kiswahili au lugha nyingine.enUdhihirikaji wa Viambajengo Katizwa katika Lugha ya KiswahiliManifestation of Discontinous Constituents in KiswahiliThesis