King'ei, Kitula Osore, MiriamOluchili, Wilson2026-04-172026-04-172024-11https://ir-library.ku.ac.ke/handle/123456789/32945Tasnifu Hii Imetolewa ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitajiya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Nov, 2024 supervisor Richard. M. WafulaUtafiti huu umechunguza usawiri wa mhusika mkinzani katika tamthilia teule za Ebrahim Hussein; Kinjeketile (1969), Jogoo Kijijini (1976) na Arusi (1980). Mhusika mkinzani ni mhusika ambaye huenda kinyume cha maadili ya jamii yake au kukinzana na mhusika nguli katika kazi ya fasihi. Katika kufanya hili, mkinzani hukuza kutoelewana au mgogoro katika utungo wa kifasihi. Malengo yaliyonuiwa kutekelezwa ni; kubainisha mbinu mbalimbali za usawiri wa mhusika mkinzani katika tamthilia teule, kuchunguza namna mhusika mkinzani anavyokuza mgogoro katika tamthilia teule na kutathmini maudhui yanayoibuliwa na mhusika mkinzani katika tamthilia teule. Nadharia mbili ndizo zilizoongoza utafiti huu; Naratolojia na nadharia ya Drama. Naratolojia iliasisiwa na Plato (1930) na kukuzwa na Rimmon-Kennan (1983), Stanzel (1984), Phelan (1987) na Keen (2003). Inahusika na vipengele vya usimulizi vikiwemo wakati, nafsi, nafasi, wahusika na maudhui. Vipengele vya wahusika na namna wanavyokuza maudhui ndivyo vilivyotufaa katika utekelezaji wa lengo la kwanza na la tatu. Naratolojia inafafanua kuhusu njia za kuwasawiri wahusika na vilevile kueleza kuhusu wahusika kama vyombo vya kuwasilishia ujumbe (maudhui). Hata hivyo, swala la ukuzaji wa mgogoro na mhusika mkinzani halielezeki vyema na nadharia ya Naratolojia. Hivyo, nadharia ya Drama iliyoasisiwa na Carl Jung (1964) ndiyo iliyotuongoza katika kutekeleza lengo la pili. Nadharia hii ya Drama inahusu matendo ya wahusika katika drama na namna yanavyopelekea kuzuka kwa migogoro. Sampuli iliteuliwa kwa mbinu ya kimaksudi ambapo tamthilia mbili; Kinjeketile na Jogoo Kijijini ziliteuliwa kimaksudi ili kuchunguza usawiri wa mhusika mkinzani kama mhusika asiyekuwepo kwenye jukwaa. Kwa upande mwingine, tamthilia ya Arusi iliteuliwa ili kuchunguza usawiri wa mhusika mkinzani kama mhusika aliyepo kwenye jukwaa. Data ilikusanywa maktabani ambapo tasnifu, majarida na makala mbalimbali yanayohusiana na mada hii yalisomwa kwa kina. Aidha data ya kimsingi ilitoka katika tamthilia teule ambazo zilisomwa na kuchanganuliwa kwa umakini na uzingativu mwingi. Hoja zinazohusiana na mkinzani zilitengwa katika mada ndogondogo, zikachanganuliwa kisha kufafanuliwa kwa maelezo yaliyoambatanishwa na dondoo mwafaka kutoka katika tamthilia teule. Jumla ya ripoti ya utafiti huu imesukwa katika sura tano. Matokeo ya kazi hii yanatarajiwa kuwafahamisha wasomi kuhusu mbinu mbalimbali za kumsawiri mhusika mkinzani katika tamthilia pamoja na nafasi yake katika ukuzaji wa mgogoro na maudhui. Utafiti uligundua kwamba, mhusika mkinzani katika tamthilia anaweza kuwasilishwa kama mhusika aliyepo kwenye jukwaa au kama mhusika asiyekuwepo kwenye jukwaa. Mhusika mkinzani anapowasilishwa kama mhusika asiyekuwepo kwenye jukwaa, huzua ukinzani kutokana na wanachokisema wahusika wengine au msimulizi kuhusu matendo yake. Haya yalibainishwa katika tamthilia za Kinjeketile na Jogoo Kijijini. Aidha, iligundulika kuwa mhusika mkinzani anapowasilishwa kama mhusika aliyepo kwenye jukwaa, huzua ukinzani kutokana na mazungumzo na matendo yake ya moja kwa moja kama ilivyobainika katika Arusi. Mbinu ambazo mhusika mkinzani amesawiriwa nazo katika tamthilia teule ni pamoja na ya kuwatumia wahusika wengine, ya kinatiki, ya kimaelezo na ya ulinganuzi na usambamba. Pia, mkinzani amebainika kuwa nguzo muhimu katika ploti ya tamthilia kwani huchochea migogoro mikuu katika drama. Mbali na hayo, utafiti umeonyesha kwamba, katika tamthilia teule, mhusika mkinzani ametumiwa na mtunzi kama chombo cha kuwasilishia maudhui makuu, kama vile udhalimu, ukatili, usaliti, siasa na utawala kwa ujumla.otherUsawiri wa Mhusika Mkinzani katika Tamthilia Teule za Ebrahim Hussein: Kinjeketile (1969), Jogoo Kijijini (1976) na Arusi (1980)Thesis