Sitiari za Kiswahili na Lubukusu: Mtazamo Linganishi

Loading...
Thumbnail Image
Date
2022
Authors
Kundu, Paul Wasike
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu unahusu matumizi mbalimbali ya sitiari katika mazungumzo ya lugha ya Lubukusu kiulinganifu na sitiari zinavyotumika katika lugha ya Kiswahili. Kichocheo cha utafiti huu ni kuwa, japo waandishi na watafiti wa fasihi simulizi hasa katika utafiti wa sitiari walitekeleza mengi katika ukusanyaji, ugawaji wa sitiari katika vitengo mbalimbali na kuzipa sitiari majukumu mbalimbali, matumizi ya sitiari katika mazungumzo ya lugha ya Kiswahili na Lubukusu kiulinganifu hayajatafitiwa. Kuna haja ya kutafiti namna tunaweza kuchanganua sitiari kiisimu katika mazungumzo ya lugha hizi mbili za kibantu kiulinganifu ili kuzifahamu sitiari zenyewe na namna zinavyotumika. Sitiari ni mojawapo ya mbinu muhimu inayotumiwa katika upashaji ujumbe katika maisha ya binadamu zinapotumiwa katika vipera tofauti vya fasihi simulizi kama methali, vitendawili, hadithi, misemo na vinginevyo ili kupitisha ujumbe kijazanda. Utafiti huu katika kujaribu kubaini matumizi haya ya sitiari kiisimu uliongozwa na nadharia ya sitiari dhanifu iliyoasisiwa na Lakoff na Johnson (1980). Wawili hawa wanaafiki kuwa, sitiari ni muhimu katika kujenga mawazo ya binadamu na lugha yao katika kila mazungumzo. Sitiari hupanga dhana mbili kijozi ambazo huenda hazifanani kiumbo au kimuundo na kuzilinganisha ili kuleta uhusiano wao. Sitiari huonyesha uhusiano kati ya dhana chanzi na dhana lengwa. Mihimili ya nadharia hii iliyoongoza uchunguzi huu ni sitiari za msimbo wa sitiari za kimuundo/konduiti, sitiari za kiorienti na sitiari za kiontolojia. Nguzo hizi zilisaidia kufahamu sababu za watu kutumia sitiari katika mawasiliano yao katika lugha ya Kiswahili na Lubukusu, aina za sitiari zinazotumika na miktadha zinamotumika. Utafiti huu ulifanywa maktabani kwa kusoma majarida, vitabu na tasnifu kuhusu sitiari, namna zilitumika, miktadha ya kimatumizi na maumbo yake mbalimbali ambayo hutupa aina zake kama data ya kimsingi ya utafiti. Aidha utafiti ulifanywa nyanjani ambapo data kuhusu sitiari ilikusanywa kwa kutumia hojaji, uchunguzi, ushiriki na mahojiano. Uteuzi wa sampuli kimaksudi ulitumiwa kwa misingi ya tajriba na maarifa ya jamii lengwa katika matumizi ya sitiari mbalimbali katika miktadha tofauti. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kuzingatia maswali, malengo na mihimili ya nadharia. Matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo na mifano. Utafiti huu umebaini kuwa sitiari hutumia ishara katika mazungumzo ya lugha ya Lubukusu na Kiswahili kiulinganifu kwa malengo mbalimbali. Imedhihirika katika utafiti huu kuwa, lugha ya Lubukusu na Kiswahili kiulinganifu huwa na miktadha sawa ya matumizi ya sitiari na malengo sawa kama kuelimisha jamii. Utafiti huu una mchango mkubwa katika kuelewa uhalisia wa sitiari na vigezo mbadala vya kuzingatiwa katika uainishaji na uchanganuzi wake.
Description
Tasnifu hii Iliwasilishwa ili Kutimiza Mahitaji ya Shahada ya Uzamili ya Kiswahili Katika Shule ya Fani na Sayansi za Kijamii, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Machi, 2022
Keywords
Sitiari, Kiswahili, Lubukusu:, Linganishi, Mtazamo
Citation