Ushairi Unaotumia Methali Kama Mlezi wa Utamaduni katika Jamii
Abstract
Makala hii inahakiki mabadiliko ya kimtindo katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa
Kiswahili. Kwa mfano, hapo awali utungo huu ulitungwa kwa kuzingatia utamaduni wa
Waswahili kama jamii. Kwa wakati wa sasa unatungwa na wasanii kutoka jamii pana ya
Afrika Mashariki. Kipengele cha methali ni miongoni mwa zile maarufu katika tungo
zilizozingatia mno arudhi za kimapokeo. Aidha, baadhi ya wasanii wanawasilisha tungo
zao kwa kuzingatia zaidi kauli mahususi wanazobuni wanatumia kwa kadri au zile teule
zinazopatikana katika mapokeo ya jamii. Katika muktadha huu, ushairi wa Kiswahili una
sifa anuwai ambazo huweza kutumiwa kuubainisha. Kwa kuzingatia au kutozingatia
matumizi ya methali katika uwasilishaji, tungo hizi zinaweza kuainishwa kimakundi.
Kwa hivyo, ushairi wa kisasa wa Kiswahili unaweza kuwa ni ule unaozingatia methali
zaidi, chache au ule unaoasi kabisa matumizi hayo. Swali ni kwamba, kati ya tungo
zinazotumia au zile zisizotumia methali katika uwasilishaji wake ni zipi zilizo bora?