Mabadiliko ya maneno ya kiswahili yaliyotolewa katika lugha ya kipsigis
Abstract
Kazi hii imenuia kuchunguza manenomkopo ya Kikipsigis yaliyotoholewa kutoka Kiswahili. Lengo hasa ni kubainisha taratibu zinazozingatiwa katika' utohozi wenyewe. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Fonolojia Leksia ambayo kimsingi hushughulikia uambishaji wa maneno.
Utafiti huu ulifanywa katika tarafa ya Longisa iliyo katika gatuzi la Bomet. Kata tatu ambazo ni Chemaner, Kembu na Kimuchul zilishirikishwa kwenye kazi hii.Tarafa ya Longisa ilichaguliwa kwa sababu inachukuliwa kuwa ingali na wazungumzaj i asili wa Kikipsigis. IIi kufanikisha kazi hii, jumla ya maneno mia moja na ishirini yalikusanywa.
Maneno yaliyochunguzwa ni nomina na vitenzi. Katika ukopaji wowote, nomino ndizo zinazokopwa kwa wingi kwa sababu ya kukosekana kwa majina ya dhana ngeni zinazozuka.
Utafiti huu ulifanywa maktabani na nyanjani. Maktabani ulihusu udurusu wa vitabu, tasnifu majarida na huduma za mtandao. Nyanjani ulihusu ukusanyaji wadata kwa kuhusisha mbinu za kushiriki, kuhoji na kurekodi. Katika kuchanganua data maneno yaliainishwa kulingana na kategoria zao na mahali pa kuambishwa.
Kwa jumla, kazi hii ina sura tano. Sura ya kwanza ni utangulizi wa kazi nzima. Sura ya pili inashughulikia muundo na maneno ya Kikipsigis. Sura ya tatu inahusu mabadiliko ya kifonolojia na ya nne inahusu mabadiliko ya kimofolojia. Mwisho ni sura ya tano ambayo ni hitimisho yenye matokeo, mapendekezo na muhtasari na utafiti. Utafiti huu una matokeo mengi hasa- mageuko ya sauti, silabi na maumbo ya maneno. Matokeo haya yana umuhimu kama inavyoelezwa kwa kina katika sura ya tano.