Uziada wa kisarufi katika Kiswahili cha wanafunzi wa Kinyala: mtazamo wa uchanganuzi linganuzi
Abstract
Lengo la kazi hii ni kuchunguza iwapo tofauti za kisarufi zilizopo kati ya Kinyala na Kiswahili ni kikwazo kwa wanafunzi wa Kinyala wanaojifunza Kiswahili sanifu. Kwa kurejelea misingi ya nadharia za Uchanganuzi Linganuzi na Uchanganuzi Makosa, utafiti huu unawalengas wanafunzi wa darasa la nane kutoka shule nne za msingi wilayani Busia (Kenya).
Kazi hii imegawanywa katika sehemu tano. Sura ya kwanza ni kitangulizi cha kazi nzima. Inashughulikia mapitio ya vitabu, mada ya utafiti, umuhimu utafiti na mbinu za utafiti.
Sura ya pili inahusu msingi wa nadharia. Nadharia ya Uchanganuzi Linganuzi inafafanuliwa kwa kuchunguza mbinu zake, upungufu wake na mihimili yake. Aidha, inalinganishwa na nadharia ya Uchanganuzi Makosa na ile ya Lugha Kadirifu.
Sura ya tatu inatoa maelezo ya kategoria nne za kisarufi zilizotumiwa. Ufafanuzi unatolewa kuhusu namna upatanisho wa kisarufi unavyojitokeza katika kila kategoria huku Kinyala kikilinganishwa na Kiswahili sanifu. Ulinganishaji wa sarufi za lugha hizi mbili unaishilia katika ubashiri wa matatizo yanayoweza kuwakumba wanafunzi wa Kinyala wanaojifunza Kiswahili kama lugha yao ya pili.
Katika sura ya nne, data iliyokusanywa nyanjani inachanganuliwa na kijadiliwa kwa tafsili. Mjadala unahusu namna uziada unavyojitokeza katika kila kategoria ya kisarufi, kama inavyoonekana katika upatanisho wa kisarufi. Mbinu wanazozitumia kuupunguza uziada huo, na kufanya makosa ya kisarufi, pia zinachunguzwa. Aidha, chanzo cha makosa hayo kinajadiliwa.
Katika sura ya tano, muhtasari wa sura za kazi hii unatolewa pamoja na hitimisho la matokeo ya utafiti kwa jumla. Vile vile, manufaa yatakayotokana na utafiti huu yanatolewa pamoja na mapendekezo kuhusu mada hii.