Tathmini ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Somo la Imla katika Shule za Upili: Gatuzi la Trans-Nzoia, Kenya
Abstract
Utafiti huu ulitathmini ufundishaji na ujifunzaji wa somo la imla katika shule za upili katika Gatuzi la Trans-Nzoia. Utafiti huu ulilenga kubainisha vipengele vya stadi ya uandishi ambavyo wanafunzi hujifunza katika somo la imla, mbinu ambazo walimu hutumia kufundishia somo la imla, changamoto zilizowakumba walimu katika ufunzaji wa imla na udhaifu uliojitokeza katika ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo na kupendekeza namna ya kuliboresha. Uteuzi wa sampuli kusudi ulitumiwa kuchagua gatuzi lililohusishwa katika utafiti huu. Shule zilizotafitiwa ziliteuliwa kwa kutumia sampuli tabakishi na bahatishi. Nadharia zilizoongoza utafiti huu ni Nadharia ya Lugha Mawasiliano iliyoasisiwa katika miaka ya 1960 na Nadharia ya Uchanganuzi Makosa ya Corder (1967). Mihimili ya Nadharia ya Lugha ya Mawasiliano ilitumiwa kuchanganua mbinu za ufundishaji wa somo la imla ilhali Nadharia ya Uchanganuzi Makosa ilitumiwa kudhihirisha vipengele vya stadi ya kuandika katika somo la imla na udhaifu katika ujifunzaji wa somo hilo katika shule za sekondari. Utafiti huu ulifanywa nyanjani. Mbinu za mahojiano na uchunzaji zilitumiwa kukusanya data. Data hiyo imewasilishwa kutumia maandishi ya nathari, majedwali na vielelezo. Matokeo yamebaini kuwa walimu wengi katika shule za sekondari wanafundisha somo la imla kijuujuu bila kufanya maandalizi ya kimaksudi. Aidha, utafiti huu umeonyesha kuwa wanafunzi wanajifunza vipengele mbalimbali vya lugha kama vile hijai, sarufi, hati bora, msamiati na matamshi bora katika somo la imla. Utafiti huu unapendekeza walimu waandaliwe warsha mbalimbali za Kiswahili ili wahamasishwe kuhusu mbinu mbalimbali za kufundishia somo la imla. Aidha, silabasi ya Kiswahili ifanyiwe marekebisho ili kuwezesha maandalizi ya kimaksudi ya ufundishaji wa imla. Isitoshe, utafiti huu unapendekeza tume ya kuwaajiri walimu (T.S.C) iwaajiri walimu zaidi na kuwaruhusu walimu wa Kiswahili kufundisha Kiswahili lugha na Fasihi pekee ili kuwapa walimu muda wa kutosha wa kufundisha vipengele vyote vya stadi za lugha.