Mchango wa fasihi simulizi katika fasihi andishi: mfano wa visasili katika Mafuta (1984) na Walenisi (1995)
Abstract
Utafiti huu ulitathmini mchango wa fasihi simulizi katika fasihi andishi. Utafiti ulilenga
kubainisha umuhimu wa visasili katika utunzi wa riwaya ya Kiswahili. Malengo ya utafiti
yalikuwa ni kuonyesha ubainikaji wa visasili, mchango na umuhimu wake katika utunzi wa
riwaya ya Mafuta (1984) na Walenisi (1995). Riwaya hizi ziliandikwa na Katama Mkangi.
Utafiti uliongozwa na nadharia ya mwingilianomatini iliyoasisiwa na mwananadharia
Kristeva (1966). Kuingiliana kwa matini katika kazi ya fasihi kuna maana ya kazi moja ya
kifasihi kuwa na sifa za tanzu nyingine ndani yake ili kupitisha ujumbe. Visasili viliteuliwa
kimakusudi kwa mujibu wa malengo ya utafiti. Utafiti ulifanywa maktabani kwa kusoma
vitabu viteule kwa kina, miswada, majarida, tasnifu na makala mbalimbali yenye data
iliyohusu mada hii. Mtafiti pia alizingatia matumizi ya mtandao ili kupata ujumbe zaidi.
Ukusanyaji wa data ulifanywa kwa kuongozwa na nadharia ya utafiti. Aidha, data
ilichanganuliwa kwa kuainishwa kwa misingi ya ubainishaji wa visasili, mchango na
umuhimu wake. Kisha, uchanganuzi wa data uliongozwa na maswali ya utafiti, malengo ya
utafiti na mihimili ya nadharia. Matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kwa mbinu ya kimaelezo
na kwa kutoa mifano mwafaka ya aina za visasili katika riwaya teule.Tunatumai kwamba
kazi hii itatoa mchango maalum kwa wanafunzi, walimu, wahakiki wa fasihi, wasomi pamoja
na wakuza mitaala kwa kuwapa mwanga zaidi kuhusu mchango wa fasihi simulizi katika
kukuza na kuendeleza uhakiki wa riwaya teule. Kadhalika, unaangazia suala la kuchanganua
visasili kama kipengele cha mwingilianomatini katika ufundishaji na ujifunzaji wa riwaya.