Grafolojia katika uchapaji wa riwaya ya mkamandume
Abstract
Utafiti huu ulichunguza mchango wa vipengele vya kigrafolojia katika uchapaji wa riwaya ya
Mkamandume ya Said A. Mohamed. Uliviangazia vipengele hivyo kwa kutathmini jinsi
vilivyotumika na athari kwa msomaji wa riwaya teule na utanzu wa riwaya kwa jumla.
Utafiti uliongozwa na nadharia ya kimtindo iliyoasisiwa na Baally (1909) na kuenezwa na
Jakobson (1958) na Halliday (1971) na kisha kuelezewa na akina Leech na Short (1981).
Aidha, mitazamo ya Leech na Short (1981) ilizingatiwa zaidi. Kulingana nao, mojawapo ya
dhana ya kimtindo inahusu matumizi ya vipengele vya kigrafolojia kama vile viakifishi,
herufi kubwa, tahajia, mlazo na hata kugawika kwa maandishi kwa aya kadha miongoni mwa
vipengele vingine vya kiisimu. Kiupeo, utafiti huu ulijikita katika riwaya ya Mkamandume,
na ulishughulikia vipengele hivyo vya kigrafolojia riwayani. Utafiti ulifanyiwa maktabani
ambamo nilisoma kwa kina vitabu mbalimbali kuhusu mada na nadharia ya kimtindo. Data
iliyokusanywa, ilichanganuliwa kulingana na malengo ya utafiti pamoja na msingi wa
nadharia ya kimtindo. Data hiyo iliwasilishwa kwa njia ya kimaelezo. Ripoti ya utafiti
ilipangwa katika sura tano. Sura ya kwanza ilijumulisha utangulizi ambamo usuli wa mada
ya utafiti, suala, maswali ya utafiti, malengo, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka,
yaliyoandikwa kuhusu mada, msingi wa nadharia, pamoja na mbinu za utafiti zilirejelewa.
Sura ya pili iliangazia riwaya ya kisasa katika miktadha ya Kimagharibi na Uswahilini. Sura
ya tatu iliihakiki riwaya ya Mkamandume huku vipengele vya kigrafolojia; viakifishi
vilivyotumika na mwandishi vikijadiliwa. Katika sura ya nne tulijadili vipengele vingine vya
kigrafolojia visivyokuwa viakifishi ambavyo mwandishi alivitumia katika ujenzi wa riwaya
huku athari yavyo ikichanganuliwa. Sura ya tano ilijumulisha ufupisho wa yaliyotangulia.
Utafiti huu ulilenga kuwanufaisha wanafunzi, wasomaji, wahakiki na wandishi wa riwaya
kwa ujumla.