Mtindo katika mashairi ya kiswahili: Aina na dhima ya kibwagizo tasnifu
Abstract
Utafiti huu umetathmini mtindo katika mashairi ya Kiswahili kwa kuzingatia dhima na aina ya kibwagizo. Mtafiti amechunguza mashairi yaliyowasilishwa kwa mitindo mbalimbali huku akitilia maanani mashairi ya Kiswahili yanayobainishwa katika matapo matatu: yale yanayozingatia mno arudhi za kimapokeo, yasiyozingatia mno arudhi (ya kati) na yale yasiyozingatia arudhi hizo (huru) ili kudhihirisha haya. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni ile ya mtindo. Nadharia ya mtindo kwa jumla inazingatia matumizi ya lugha kwa kutathmini maana ya kijuujuu katika ruwaza ya sentensi au mfumo wa neno ili kubainisha au kufasiri maana fiche. Tasnifu hii imegawanyika katika sura tano: sura ya kwanza ni utangulizi ambapo mada ya utafiti, madhumuni ya utafiti, sababu za kuchagua mada na upeo wa utafiti zimeshughulikiwa. Pia, udurusu wa maandishi yanayohusu mada hii pamoja na nadharia iliyoongoza utafiti huu imejadiliwa. Sura ya pili imechanganua namna watunzi wa mashairi ya kimapokeo wanavyokitumia kibwagizo. Sura ya tatu imechanganua namna kibwagizo kinavyotumika katika mashairi ya kati ilhali sura ya nne imeshughulikia mashari huru ya Kiswahili. Sura ya tano ni hitimisho ambapo muhtasari na matokeo ya utafiti umeshughulikiwa pamoja na mapendekezo ya
Utafiti.